DHANA YA MOTIFU KATIKA RIWAYA INAVYOJADILIWA NA WATAALAMU WA KISWAHILI
Motifu
ni kati ya vipengele muhimu katika uchambuzi wa kazi za kifasihi, hususani
katika kuchambua vipengele vinavyojenga maudhui ya kazi hizo. Dhana ya motifu
imefasiliwa na wataalamu mbalimbali. Kwa mfano: Dorson (1972) kama
alivyomnukuu Thomson (1932:32) anasema motifu ni kizio kidogo thabiti
kipatikanacho katika sanaa jadia, maelezo ambayo masimulizi yote
yanajinasibisha nayo. Yanaweza kujikita kwa mhusika fulani ndani ya masimulizi,
ndani ya matendo yaliyo katika masimulizi na mara nyingine katika hali
inayojitokeza sana
katika tendo lililo ndani ya usimulizi.
Thomson
naye aliangalia motifu kwa kuihusisha kwa kiasi kikubwa na masimulizi ndani ya
sanaa jadia. Hakuangalia motifu kwa mapana yake katika kazi zote za fasihi
andishi na simulizi.
Wamitila
(2003) kwa upande mwingine anasema dhana hii, motifu, hutumiwa kurejelea wazo
kuu na sehemu ya dhamira katika kazi ya kifasihi. Huweza pia kutumiwa kuelezea
elementi ya kimuundo au kimaudhui inayotawala kazi fulani. Anatoa mfano wa
riwaya yake iitwayo Binaadamu ambapo
anasema safari ni motifu muhimu ya kimuundo na kimaudhui.
Umuhimu
wa motifu anaouelezea Wamitila kwa kuzingatia maudhui na muundo unamaanisha
kwamba, kuwapo kwa motifu ya safari katika hadithi hiyo ndiko kunakobeba muundo
na maana ya hadithi. Motifu hiyo haiwezi ikaondolewa kwani itaathiri muundo na
ujumbe au maana ya hadithi hiyo.
Encyclopedia
the Free Dictionary (2011) inasema motifu ni kitu, jambo, wazo au muundo katika
kazi ya fasihi linalojirudiarudia. Motifu ni muhimu kwa sababu inamwezesha mtu
kuona mawazo makuu na dhamira anazojaribu kuzionyesha msanii ili aweze
kuitafsiri kazi ya sanaa kwa ufasaha zaidi.
Mulokozi
(2009) anayaendeleza mawazo ya Encyclopedia (imeshatajwa) na kusema motifu ni
kipengele radidi cha kijadi/kikaida au kimaudhui kinachotumiwa na wasanii
katika kazi zao ili kutoa ujumbe fulani. Mulokozi (keshatajwa) anatoa mifano ya
motifu za kifasihi kuwa ni: motifu ya mama wa kambo, motifu ya safari, motifu
ya msako, motifu ya mwanamke mshawishi, motifu ya bi kizee, motifu ya mzungu
mweusi, motifu ya mtoto wa ajabu, motifu ya mtoto kigego, motifu ya mnyonge
anayemshinda mwenye nguvu, motifu ya nunda/ zimwi mla watu, motifu ya mwali
aliyekataa kuolewa pia motifu ya taksiri (Achilles’ heel).
Kwa
kuzingatia umuhimu wa motifu katika kazi za fasihi, aidha kwa kukusudia au bila
kukusudia, waandishi wengi wa kazi za fasihi wamekuwa wakijumuisha motifu
katika uandishi wa kazi zao. Motifu nyingi zinajitokeza moja kwa moja au
kisitiari katika kazi hizo.
Motifu
za msako na safari ni kati ya motifu zinazojitokeza kwa kiasi kikubwa sana katika kazi za
fasihi. Hii inaweza ikachangiwa na ukongwe wake kama
fasihi yenyewe. Kama anavyosema (Senkoro
1997:11)
Kuna ukweli wa tangu kale wa kifasihi
ambao unasisitiza kuwa roho ya kazi yoyote ya kifasihi iliyo bora ni safari. Na
ni kweli motifu hii ni ya kale kama fasihi
yenyewe.
Motifu
za safari na msako kwa kiishara zinahusiana na hatua za makuzi za wahusika
katika kazi za fasihi. Kama Senkoro (1997) anavyoiangalia motifu ya safari
katika mitazamo mbalimbali na mmojawapo ukiwa “safari kama
ishara ya mchakato wa makuzi.”
No comments:
Post a Comment